Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akidai kuwa
hali ya chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya, Serikali
imesema hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za
wastani.
Zitto alidai jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya
chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na
chakula cha kutosha miezi miwili.
Kwa mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba
inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), imebaki
na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni cha kutosholeza siku
nane.
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba
alijibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha kutosha wala
siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo
ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi
kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo
wakala haukununua chakula kingi.
“NFRA inanunua chakula kwa kuangalia mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu
wakivuna sana maghala yao yanakuwa yamejaa na mahitaji ya chakula
yanakuwa madogo ndiyo maana Serikali hainunui chakula kingi. Miaka
miwili iliyopita Serikali ilinunua mahindi kwa wingi lakini yaliishia
kuharibika,” alisema Dk Tizeba.
Aliongeza kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga ghala jingine lenye
uwezo wa kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa lenye uwezo wa
tani 246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya 500,000.
“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko watavuna kama
kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi bila
vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo siwezi kutaja
kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila kinatosha siyo
kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” alisema Tizeba.
Juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani katika kata ya
Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema kauli ya Rais
John Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba Serikali haina
shamba ni kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa akiba ya chakula
ya kutosha.
Alidai kuwa hali ya chakula nchini si nzuri, wananchi wanashuhudia namna
bei za vyakula zinavyopanda kila siku akidai kuwa bei ya sembe na
mchele zimekuwa juu na gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na
uhaba wa chakula kuwa mkubwa.
“Hali ya chakula inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya
Serikali kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma
zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa
chakula hicho kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi
kumudu gharama za chakula,”alisema Zitto.
Aliongeza kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za chakula wakati kipindi
kama hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa na tani 459,561.
Takwimu alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika ripoti ya BoT ya
Novemba mwaka jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016 hadi Julai
2016, akiba ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi 49,632, lakini
hadi Oktoba mwaka huo iliongezeka hadi 90,476.
Ripoti hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa chakula kwa mwaka jana na
miaka mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014 Januari, kulikuwa na
tani 235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka 2015 Januari
kukiwa na tani 459,561 na Desemba 180,746.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania
(Mviwata), Steven Ruvuga alisema hali halisi kwa wakulima siyo nzuri kwa
kuwa mvua zilinyesha chini ya kiwango, hivyo kuna hofu ya ukosefu wa
chakula cha kutosha baadaye.
“Sasa hivi nipo Kiteto na kwa kawaida mahindi yalipaswa kuwa tayari
yameinuka kufikia walau mabega ya mtu mzima, lakini nikiyatizama sasa
bado yako chini.
"Mwaka huu kuna hatari ya ukosefu wa chakula na naishukuru Serikali kwa
kuwa imeanza kuchukua hatua katika maeneo yenye uhitaji,” alisema
Ruvuga.
Aliongeza kuwa Ghala la Taifa linapaswa kuwa na wastani wa tani 300,000
za akiba lakini kama sasa zipo 90,476 zinaweza zisikidhi mahitaji ya
kila mtu hivyo ni vyema ikabuni mpango mbadala
Home / featured /
kitaifa /
zitto
/ ZITTO Kabwe Adai Kuna Uhaba Mkubwa wa Chakula Nchini.........Waziri wa Kilimo Ampinga
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.