Familia moja jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa
kike wa miaka mitatu katika kaburi lililofichwa, huku majirani
wakidanganywa kuwa binti huyo yupo hai.
Taarifa za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama.
Kwa sasa kuna mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru
Losipha aliyezikwa kwa siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi
zaidi.
Inadaiwa kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au
ukeketaji na ngariba, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku
familia yake ikishuhudia.
Kitendo hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti
wilayani Arumeru Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku
tatu tu, kabla ya mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu,
hajaingia mwaka mpya wa 2017.
Mtendaji wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na
taarifa hizo hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa
uchunguzi na ndipo alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo
cha Polisi cha Ngaramtoni.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na
liwe na kwamba ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo
asiye na hatia, uchunguzwe upya.
“Ndio kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha
mahakama ili twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli
mtoto huyo amezikwa humo na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza
uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema Kamanda arles Mkumbo.
Baba wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki
kutokana na ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi
kirefu kabla ya kupoteza maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai
yake hayo yanapingana na ripoti ya muuguzi katika duka la dawa lililopo
kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.
“Walimleta mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na kutokwa na damu nyingi,”alidai.
Muuguzi huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo zilipomfikia.
Huku serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado
kuna familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya
Ziwa, zinaendeleza mila hiyo kwa siri.
Kwa sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana, kuepuka kukamatwa.
Ngariba wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe
wasiokuwa na ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo
husababisha uvujaji mwingi wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya
magonjwa mengine.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.