Viongozi wa Haras El Hodoud wameshindwa kukamilisha
kwa wakati taratibu za usajili na kujikuta wakimkosa mshambuliaji huyo
mwenye kipaji cha hali ya juu kutoka Simba
Ajibu ameiambia Goal, alikuwa na matumaini makubwa ya kutua Misri, lakini sasa ndoto zake zimefutika baada ya timu hiyo kushindwa kuharakisha taratibu za usajili wake.
“Wenyewe ndio waliochelewa kukutana na uongozi wa Simba, ambao ndiyo wananimiliki, lakini mambo yote yalikuwa sawa ikiwemo kukubaliana mshahara inaelekea kama kutokamilika kwa sasa,” amesema Ajibu.
Mshambuliaji huyo mwenye kipaji cha hali ya juu amesema kwa sasa matumaini yake ni kusikiliza ofa ya Kaizer Chief ambao walionyesha nia ya kumsaliji bila ya majaribio kutokana na kuvutiwa na kipaji chake.
Angban aitabiria Simba Ubingwa
Ajibu amesema anamsikilizia wakala wake kama wanaweza kulifanikisha dili hilo kipindi hicho kama ikishindikana atabaki msimbazi kwa ajili ya kuisaidia timu yake kupata ubingwa wa ligi ya Vodacom wakiwa wanaongoza.
Jana uongozi wa Simba kupitia kwa Katibu Mkuu Patrick Kahemela, alikiri kuwa mchezaji huyo alifuzu majaribio hayo na walikuwa kwenye mkao wa kupokea ofa kutoka timu mbili za Hodoud na Chief, lakini pande zote mbili zimekuwa kimya na hawaoni haja ya kuwastua kwa sababu wao ndiyo wenye shida na mchezaji.
Msemaji wa timu hiyo Hajji Manara ameiambia Goal, kuwa baada ya mpango huo kuonekana kukwama tayari mchezaji huyo wamempeleka Zanzibar ambapo kikosi chao kipo kwa ajili ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Ajibu alialikwa na klabu ya Hodoud, kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki moja na kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo mchezaji huyo alifanya vizuri na kufanikiwa kumshawishi kocha lakini viongozi wa timu hiyo walichelewa kukamilisha taratibu za usajili hadi siku ya mwisho ya usajili mdogo.