Yanga wanakabiliana na Lyon, wakiwa katika nafasi ya pili na pointi 36, huku Lyon wakiwa nafasi ya 11 na pointi zao 14
Kikosi cha Yanga kesho kitakuwa na kibarua cha kuusaka uongozi wa ligi wakati itakapoivaa African Lyon kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi iliyopita na kufanikiwa kukaa kileleni kwa muda kabla ya kutolewa na Simba Jumapili.
Mabingwa hao watetezi wanakwenda kukabiliana na Lyon, wakiwa katika nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 36, huku  Lyon wakiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo na pointi zao 14.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, hivyo ni wazi Lyon hawatokubali kupoteza pointi zote sita kwa Yanga msimu huu.
Lyon pamoja na kuwa moja ya timu zilizofanya vibaya kwenye mzunguko wa kwanza, lakini imejiwekea rekodi ya pekee, baada ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga vinara Simba lakini ndiyo timu ambayo imeweza kuilazimisha sare timu tajiri ya Azam katika michezo yote miwili licha ys timu hiyo kujaa mastaa wakigeni kutoka mataifa ya Ghana na Cameroon.
Kikosi cha Yanga kitaingia kwenye mchezo wa kesho huku kikitoka kwenye mgomo wa wachezaji waliokuwa hawajalipwa mishahara yao ya mwezi Novemba na kusababisha kushindwa kufanya mazoezi kwa siku mbili.
Tayari uongozi umeshamaliza tatizo hilo na timu ilirejea mazoezini jana asubuhi na jioni na leo wamefanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo huo wa kesho lengo la kocha Lwandamina ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuwapa presha Simba wanaoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili.
Katika mchezo wa kesho kocha Lwandamina anatarajia kumuanzisha kiungo mpya aliyemsajili kwenye dirisha dogo Justine Zullu maarufu kama ‘Mkata Umeme’  ambaye alikosa mchezo wa kwanza baada ya kutokuwa na kibali cha kufanyia kazi.
Kikosi cha Lwandamina hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa na kile kilichoanza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu, na ataendelea kumtumia nahodha wake Haruna Niyonzima kama mchezesha timu ili kupata mabao.
Simon Msuva ambaye alifunga mabao mawiili kwenye mchezo uliopita anatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza sambamba na Donald Ngoma na Hamis Tambwe ambao mchezo uiopita walitoka kappa licha ya kupata nafasi nyingi za kufunga.
Kocha huyo ataendelea kuutumika mfumo wake wa 4-3-3, ambao umekuwa ukimpa mafanikio tangu akiwa anaifundisha Zesco United ya kwao Zambia na kuifikisha kwenye nusu fainali ya klabu bingwa Afrika.
African Lyon wao pamoja na kuwasumbua Azam katika mchezo uliopita na kulazimishwa sare ya bila kufungana lakini hawapewi nafasi kubwa ya kuwasumbua Yanga ambao wanaonekana kuwa na mifumo mingi ya kiuchezaji ambayo imekuwa ikiwasaidia kupata matokeo.
Tegemeo kubwa la Lyon ni kipa wake raia wa Cameroon, ambaye alionyesha kiwango cha juu na kuwabania Azam ambao walikuwa wakiwatumia nyota sita wapya walio wasajili kwenye dirisha dogo.